BAADA ya kutangazwa kwa wasanii
wa muziki walioingia kwenye kinyang’anyiro cha tuzo za muziki wa Tanzania yaani
“Kilimanjaro Tanzania Music Awards” Aprili 25 mwaka huu, mwanamuziki Farji Nyembo
‘Ommy Dimpoz’ anaonekana kwenye vipengere 7 vya tuzo hizo. Hiyo ni baada ya
takribani siku 5 tangu zilipotangazwa tuzo za muziki wa nchini Ghana
zijulikanazo kama Vodafone Ghana Muzic Awards ambazo zimezinduliwa Aprili
20 mwaka huu.
Katika tuzo hizo za nchini Ghana, kundi la
muziki lenye wanamuziki wawili Paedae na Mugeez, linalojulikana kama R2Bees
ndilo lililoongoza kwa kutajwa mara nyingi zaidi kwenye vipengere vya tuzo
hizo. Jina la kundi hilo limetokea kwenye vipengere 8 ikiwa ni pamoja na kipengere
cha wimbo bora wa mwaka, kipengere ambacho Ommy Dimpoz pia ameingia kwa tuzo za
muziki za hapa nchini Tanzania. Pia mmoja
wa wanamuziki wa kundi hilo anayeitwa Mugeez ameingia kwenye vipengere
vya msanii bora wa kiume na mtunzi bora wa mashairi, sawa na Ommy Dimpoz kwenye
msanii bora wa kiume kwa ujumla na mtunzi bora wa mashairi wa Bongo Flava.
Ommy Dimpoz ni miongoni mwa
wanamuziki wa nchini Tanzania wanaofanya vizuri na tayari ameanza kujitangaza
kimataifa kwa kurekodi nyimbo za kushirikiana na wanamuziki mbalimbali barani
Afrika akiwemo J.Martin wa Nigeria.
Kama mdau wa muziki na msimamizi
wa Blog ya Datsongwritertz, namshauri Ommy Dimpoz kurekodi wimbo na kundi hilo la nchini Ghana.
Katika tuzo za muziki za mwaka huu nchini Ghana, R2Bees wanashindanisha wimbo
wao wa Life (Walahi) na nyimbo za wakali wengine kama Azonto Fiesta wa Appietus,
Sarkodie na Kesse, Antenna wa Fuse ODG na nyimbo zingine kwenye kipengele cha
wimbo bora wa mwaka. Katika kipengere hicho kwa tuzo za muziki za Tanzania, Ommy
Dimpoz anashindanisha wimbo wa Me n U aliomshirikisha mwanadada Vanessa Mdee na
nyimbo zingine kali ambazo ni Dear God ya Kala Jeremiah, Leka Dutigite ya
Kigoma all stars, Mapito ya Mwasiti akimshirikisha Ally Nipishe na Pete ya Ben
Pol.