Mmoja wa majeruhi wa bomu la shule ya msingi Tumaini 1994, Datius Kalokola hospitalini na baada ya kurudi nyumbani
Ni kichwa cha habari iliyotoka
kwenye gazeti flani siku ya alhamisi tarehe 1 Septemba 1994, siku moja baada ya kutokea mripuko wa bomu katika shule
ya msingi Tumaini iliyoko Manispaa ya mji wa Bukoba. Ilikuwa Jumatano 31 Agosti 1994 majira ya saa mbili asubuhi tarehe kama ya leo, tulipowapoteza wanafunzi wanne huku 85 wakiwa wamejeruhiwa kutokana na
ajari hiyo. Nianze kwa kuwakumbuka wenzetu waliotutoka siku hiyo. Mungu azilaze roho zao mahali pema peponi Ibrahim Mebu, Salehe Abdalah,
Yusuph Bahati na Emmanuel Joseph.
Tukiwa tumejipanga mistari “parade”
tayari kukaguliwa ili tuanze gwaride kuelekea madarasani, mara nikasikia kishindo
kikubwa kilichoambatana na hali ya mtikisiko. Hali iliyomfanya kila mwanafunzi
akimbie pasipo kujua jambo gani limetokea. Baada ya kukimbia umbali wa
takribani mita 15 kutoka eneo la tukio ghafra nikahisi kuishiwa nguvu mguu
wangu wa kushoto, niliposimama na kugeuka nyuma nikaona idadi ya wanafunzi
wasiopungua sita wakiwa wamedondoka chini eneo la tukio.Nilipotizama mguu wangu
ulikuwa ukitokwa na damu nyingi.Nilipata mshtuko na mshangao mkubwa huku nikiwaona wanafunzi wengine pia
wamejeruhiwa sehemu mbalimbali za miili yao. Walimu walitahamaki wasijue
wafanye nini zaidi ya kutuambia wanafunzi tuliokuwa bado tuko ndani ya
mazingira ya shule tulale chini. Wakati huo wengi wetu wakiwa hawaonekani
kabisa katika mazingira hayo ndani ya muda mfupi wengine pasipokujua kama
wamepatwa na majeraha na wengine wakikimbia kuelekea nyumbani kwao huku wakilia
sana na damu zikiwatoka.
Nikiwa kwenye gari l a Msalaba
Mwekundu na majeruhi wengine kuelekea
hospitali, tulikutana na baadhi ya wanafunzi wakirudi shuleni baada ya kufika
nyumbani na kugundua hawako pamoja na ndugu zao ambao walikuwa nao shule moja.
Hali ya utulivu ilipotea ghafla ndani ya mji wa Bukoba na hasa kutokana na
taarifa zilizowafikia wazazi wa
wanafunzi ambao walikuwa wakijiandaa kwenda kazini na wengine wakiwa tayari
wamefika maeneo yao ya kazi. Hakuna mwanafunzi wa shule ya jirani aliyesubiri
kupewa ruhusa ya kwenda nyumbani na mwalimu wake hasa pale wanafunzi wa shule
ya msingi Tumaini walipoonekana wakipita karibu na shule hizo wakibubujikwa machozi huku wakiwa na alama za damu kwenye
mashati na magauni yao ya shule na wengine wakitoa taarifa kwamba ndugu zao au
marafiki zao wamepoteza maisha kwa sababu hawaonekani.
Tukiwa katika chumba maalum
kilichoandaliwa kwa ajiri ya kupokea majeruhi wa ajari hiyo, dakitari
alimwambia nesi mmoja amtizame mwenzetu ambaye aliletwa akiwa hajitambui.Alikuwa
amelazwa chini pembeni yangu. Baada ya nesi huyo kutekeleza agizo hilo kwa
kutumia kipimo ambacho alimuwekea kifuani, nilishuhudia mama huyo nesi akimwaga
chozi bila kujizuia. Kumbe huo ndiyo ulikuwa mwisho wa kijana mpole Yusuph
Bahati amabaye tuliwai kuishi jirani maeneo ya Kashai. Wakati huo nimeshafahamu
kwamba kilichotokea ni mlipuko wa bomu.
Jioni ya siku hiyo baada ya
kutolewa kwenye chumba cha upasuaji ndani ya Hospitali ya Mkoa Kagera, nilijikuta ndani ya wodi namba 4 ya
hospitali hiyo pamoja na wanafunzi wengine wengi.Wodi mbili za hospitali hiyo
ambazo ni wodi namba 4 na namba 5 zilipokea majeruhi wa ajali hiyo na wagonjwa
waliokuwa humo kabla ya ajari wakahamishiwa vyumba vingine. Nakumbuka tulilazwa
wanafunzi wawiliwawili kitanda kimoja kwa siku hiyo ya kwanza. Kupitia maongezi
ya siku hiyo, nikafahamu kwamba wametutoka wenzetu wanne kutokana na ajari hiyo
akiwemo Ibrahim Mebu ambaye alifariki papo hapo.Huyu pamoja na mwingine
aliyeitwa Salehe Abdarah tulikuwa wote darasa la nne, wakati Yusuph Bahati na
Emanuel Joseph wakiwa darasa la tano.
Kutokana na maelezo yaliyotolewa
na baadhi ya wanafunzi ,bomu hilo liliokotwa jalalani na mwanafunzi mmoja
ambaye hakufahamika kwa jina, akamuuzia
Ibrahimu Mebu shilingi ishirini, wote pasipokujua kama ni kitu cha hatari.
Ibrahimu alikaa nalo kwa takribani siku saba akija nalo darasani na kurudi nalo
nyumbani kabla halijaripuka.Kilichosababisha bomu hilo kuripuka ni baada ya
kulifungua ikiwa ni katika hali ya michezo pasipo kujua ni kitu gani kitatokea.
Shukurani za dhati ziwaendee
wafanyakazi wa Hospitali ya Mkoa wa Kagera na Bugando ya Mwanza kwa jinsi
walivyojitoa usiku na mchana kuhudumia majeruhi na hasa wale waliokuwa na hali
mbaya sana akiwemo Benedict Nshegize. Nawashukuru pia askari wa jeshi la ulinzi
waliofika shuleni hapo kuwaonesha wanafunzi aina na maumbo tofauti ya vitu vya
hatari kama hivyo ili wanafunzi wasivisogelee pindi wavionapo na ikibidi kutoa
taarifa mahali panapotakiwa. Shukurani kwa mkuu wa mkoa aliyekuwepo kwa kipindi
hicho Mzee Philip Mangula kwa ukaribu na msaada aliyoutoa, wazazi, walimu na
wanafunzi wa shule ya msingi Tumaini na shule za jirani.
Kama msimamizi wa gazeti tanzu
hili la Semadat (Semadat Blog) na mwandishi wa kumbukumbu hii ,nikiwa pia miongoni mwa waliokuwa majeruhi wa ajari hiyo,
natoa shukurani za pekee kwa wazazi wangu, baba yangu mzazi Mzee Felix Kalokola
ambaye kwa sasa ni marehemu, mama yangu mzazi Bi.Philotea Kalokola, Baba mkubwa
Mzee Petro Buberwa na mjomba wangu maarufu kama
Dr.Lugenga, wa Hospitali ya Mkoa Kagera. Pia namkumbuka babu yangu
marehemu Philadelph Kamanzi ambaye aliendesha baiskeli jioni ya siku hiyo, akiwa
na huzuni kubwa kutoka Kijijini Kasharu na kufika mjini Bukoba usiku baada ya
kupata taarifa ambazo ni tofauti kidogo kwamba bomu hilo limeangamiza wanafunzi
wote wa shule ya msingi Tumaini.
Sina cha kuwalipa ndugu na marafiki zangu mlionipa huduma kwa kipindi
cha takribani miezi miwili nikiwa hospitalini hatimaye nikapona na kurudi
shule, hata nikaweza tena kuungana na wanafunzi wenzangu kucheza mpira muda wa
mapumziko.
Namshukuru Mungu na namuomba
awasaidie wanafunzi wote Tanzania, Afrika na Ulimwengu mzima, hasa wa shule za
awali na msingi kuepukana na majanga kama haya.
Miaka 7 mpaka 10 baada ya tukio hilo (Kidato cha nne na cha sita)
KWELI KUMBUKUMBU NI MUHIMU SANA, NA HAPA NDIPO MTU UNAPOKUJA KUONA UMUHIMU AU KAZI YA FASIHI ANDISHI KATIKA JAMII, KWANI TUKIO HILI LIMETOKEA MWAKA 1994 MPAKA LEO HII 2013 NI MIAKA TAKRIBAN 19 IMEPITA, ASANTE SANA DATIUS HAKUNA KATI YETU ALIYEELEWA KAMA TULIKUWA PAMOJA SHULE YA MSINGI TUMAINI NA TUKAKUTANA TENA IFM BILA KUJUA MPAKA TUMEACHANA NDIPO TUNAKUJA KUFAHAMU, SHUKRANI NYINGI ZIMUENDEE MJWAHUZI LUKAMBUZI KWA KUFUNGUA GROUP YA TUMAINI PR. SCHOOL AMBAYO NDIYO ILIYOFICHUA HABARI HII.
ReplyDeleteNi kweli unavyosema Juma.
ReplyDelete