UA-45153891-1

Wednesday, November 27, 2013

MAKOSA 5 YA KIMASOKO YANAYOFANYWA NA WASANII KUHUSU MITANDAO YA KIJAMII NA JINSI YA KUYAREKEBISHA

Maoni ya semadat blog


AY, Miongoni mwa wanamuziki wa nchini Tanzania wanaotumia vizuri nafasi ya mitandao ya 
kijamii kujitangaza


1. Kutoingia kabisa: Msanii hasipoingia katika ulimwengu huu wa mitandao ya kijamii anakosa nafasi muhimu ya kujitangaza mwenyewe. Japo wengine husema hawana muda au hawawezi kutumia hii teknolojia, kuna haja ya kuingia japo dakika 30 tu kwa siku ndani ya mitandao hii.

Tafuta mtu wa  kukusaidia ambaye atafanya yote yanayotakiwa kufanyika kila unapohitaji kufanya hivyo. Kama tatizo ni muda, basi afanye hivyo badala yako kwa muda ambao haupo na kama  tatizo ni kutoweza kutumia, awepo muda wote wakati huo ukijifunza taratibu.


2. Kuingia tu pasipo kutumia:  Kuwa kwenye mitandao ya kijamii na kuweka taarifa zako, kwa mfano wewe ni nani, unafanya nini, njia ya kukupata n.k, ni mambo muhimu zaidi, lakini lazima pia kila unaporudi  uwe na sababu.

Hakikisha unakuja na jambo lolote, kama ni taarifa au jambo lolote la kuwafanya watu wajue kinachoendelea kuhusu wewe, wasanii wengine au matukio mbalimbali.


3. Kutofanya kama unavyotaka kufanyiwa: Ukiuliza ni wangapi wanasema asante kwa watu waliowafuata kwenye mitandao yao ya kijamii utapata mmoja kati ya mia moja. Pia ni wachache sana huwafuata wengine badala ya kungoja wafuatwe kwenye Facebook, Twitter au Instagram na mitandao mingine.

Mitandao ya kijamii ni kwa ajili ya mawasiliano na uhusiano, pia ni vyombo ya kujitangaza kwa njia ya mtandao wa intaneti. Ukijenga uhusiano mzuri utawaweka mashabiki wako karibu na wewe zaidi. Pia ni vizuri wakati mwingine kuzungumzia mambo mengine na wasanii wengine tofauti na kazi zako, kuwatangaza wasanii wengine, kuwashauri na kuwakosoa itakuongezea mashabiki wengine kutoka kwao.


4. Kuhama mitandao badala ya kuongeza: Wapo wanaozani mitandao ya kijamii ni fasheni. Kila mtandao una faida zake na mapungufu yake, ndiyo maana kila kukicha inaibuka mingine ili kuziba mapengo lakini haimaanishi kwamba  ndiyo bora zaidi.

Jitaidi kuwa sehemu nyingi kwa kadri inavyowezekana, pia ongeza ufahamu juu ya mitandao hii.Ukifanya hivyo utaelewa umuhimu wa kila mtandao, umaarufu wake na matumizi yake. Husiondoke Facebook kwenda Instagram, badala yake endelea kuwa FB na fungua akaunti ya Instagram pia. Huu ni mfano.


5. Kutofikiria kama ‘Brand’: Hapa namaanisha jina linalofahamika kibiashara au lenye lengo la kufahamika kwa ajili hiyo. Jina la msanii ni kama jina la kampuni, taasisi, mkoa au nchi. Baadhi ya wasanii hutumia mitandao ya kijamii kama mtu yeyote mwenye lengo tu la kujenga mtandao na marafiki zake kwa ajili ya kupashana habari na kuwasiliana kwa ujumbe mfupi wa maneno.

Si vizuri kutumia majina tofauti kwenye mitandao ya kijamii, kama jina lako ni ‘Christmas Day’ na ndilo jina unalotumia Facebook, kwenye Twitter, husitumie ‘Christmas Eve’. Kumbuka kuwa na rangi zako kama ilivyo Bendera ya Taifa, Nembo ya Taifa au ya kampuni, ili zitumike kujenga uhusiano kati ya mitandao ya kijamii unayotumia, picha za kurasa za mwanzo za mitandao hiyo zisiwe na tofauti sana. Pia ni muhimu kuzingatia fursa zinazotolewa na baadhi ya mitandao kutofautisha matumizi ya kawaida na ya kibiashara. Kwa mfano, hata Facebook watashangaa kama unatumia akaunti kujitangaza badala ya kuwa na akaunti alafu ndani yake ukafungua ukurasa maalum kwa ajili  hiyo yaani ‘Facebook Page’.

Wema Sepetu, msanii wa Filamu nchini Tanzania ambaye pia anatumia vizuri fursa ya mitandao ya kijamii

Amanda  Bynes, muigizaji wa nchini Marekani anayetajwa kama miongoni mwa watumiaji wazuri wa mitandao ya kijamii  katika kazi zake za sanaa

 Amanda Bynes

2 comments:

  1. Hiyo ni kweli kabisa wasanii wengi wanapenda kutumia majina tofauti tofauti ktk mitandao ya kijamii hivyo inakuwa tabu katika kujitangaza.

    ReplyDelete